Wednesday, December 28, 2005

Asalam aleikum

Asalaam aleikum waungwana wote waandishi na wasomaji wa blogu za Kiswahili na nyinginezo. Ama hakika mvuvumko wangu leo waanzia hapa kwenye jukwaa hili la kupashana na kujadili habari na masuala anuai. Bila ya kuchelewa, nimekuwa nikicheza ngoma hii kwa kutazama na kukodolea macho nikiwa nimejikunyata pembezoni mwa kiwanja (wengine husema uwanja). Yawezekana kabisa baadhi yenu mmepiga chabo nomino langu likitokea katika kuchangia hili ama lile.

Awali ya yote mie ni miongoni mwa wale tunaosapoti 'blog' ziitwe 'blogu', 'blogger/bloggers' tuite 'wana/mwanablogu.' Au mwasemaje. Niliwahi kuchangia hili la neno la blog kwa Kiswahili katika blogu ya Jeff. Baada ya kuwa nimefanya hivyo nikabahatika kuendelea kufanya utafiti wa maneno mengine ambayo tumebomu kutoka viluga vingine. Nimefanikiwa kupta maneno ya wingi wa haja tu lakini leo nitawapa moja ambalo limenishangaza kwa kweli. Jamani lugha haibadiliki kama tarehe. Kumbe hata neno 'bamia, ile mboga inayoteleza mdomoni, tulilitoa uarabuni!

Boniface Makene amekuwa haishi kunipemba eti nami nijiunge kilingeni. Kuandika na kuandika-andika havitangamani. Ndesanjo naye hakua kando katika kushadidia hamasa hii niliyokua nayo dahari za siku nyuma ingawaje msongo wa shule na kazi na mambo kadha wa kadha vilifanikiwa kunivuta nyuma. Hayawi hayawi, basi yaelekea sasa yanaweza kuwa yanakua.

Kutamani kuwa na ka-blogu kangu na kuweza kukafanya kadumu ni vitu viwili tofauti. Kumbe kwa kuwa maji nimeshayavulia salawili basi sina haja ya kuyachumpia ili kuyaogelea. Si haba nanyi sasa mwaweza kuwa mkipata pahala pa kutembelea japo mara moja kwa muda fulani.

Twende Kazi