Sunday, January 01, 2006

Nimekula Ugali Alabama

Tangu nilipopata ufahamu wa kutambua jema na baya, nimekuwa na njozi ama ndoto za aina aina. Nikiwa mdogo bila shaka nilianza kufikiri kuwa mtu fulani hapo nitakapokuwa mtu mzima (ukiwa mdogo unakuwa kipande?). Kama mtu mwingine yeyote wakati huu mtu hufikiria mathalani kuwa daktari, mwalimu, dereva, askari polisi na kadhalika. Pia wakati mwingine hufikiria kupata vipawa na uwezo wa kufanya mambo kadhaa pale wasaa utakapowadia mfano kuoa ama kuolewa, kupata watoto ama hata kusafiri kwenda mikoa hata nchi za mbali.
Baada ya njozi zangu za utotoni na ujanani kutokea kweli na zingine kubakia kuwa za alinacha tu, hatimaye ile ya kisafiri nchi za mbali ilitimia mwaka tulioumaliza hivi punde pale mwezi wa tano nilipoletewa mkataba Mbeya ili niusaini kukubali ama kukataa kuja hapa kwa Mzee Joji kudurusu Kiswahili. Kama ilivyo kwa wa-Bongo wengi wasaa wa kuja Marekani hufuatia ule wa kwenda mbinguni kwa umaarufu. Nani akatae kuja Mtoni? Nikiwa na mchanganyiko wa bashasha na huzuni ya kuiacha kazi ya kufundisha kule nyumbani Mbeya, hatimaye nilikanyaga udongo wa wababe wa dunia pale mwezi wa nane. Nikiwa na shauku ya kukuta mambo mema mengi hapa Marekani, kwangu ulikuwa wakati mgumu kuiacha kazi niliyokuwa nimeizoea na marafiki zangu wa haja. Sikukumbuka hata kumuaga bibi yangu Ndimbumi Kafwila kule Kyela. Mungu awalinde hata tutakapokutana tena.
“La haula lakwata! Kumbe Marekani iko hivi!” Ndiyo yaliyokuwa maneno nilijisikia kuyasema pale ile ndege iliyoninyakua Afrika ya Mzee Mandela ilipokuwa ikielekea kutua jijini Atlanta. Kama watu wengi wadhaniavyo, hakika mandhari ya nchi hii yalisema karibu ndugu Mwaipopo hapa Mtoni ufurahie kutokuwepo kwa mbu na inzi, ufurahie barabara za orofa, umeme na maji visivyokatika kama Dar es Salaam anakokaa Boniface Makene na Muhidin Issa Michuzi. Hakuna haja ya kuyaorodhesha sana maajabu ya hapa Marekani.
Nikawa katika “nchi ya ahadi" katika jimbo la New Jersey. Siku ya kwanza mgahawani nikashangaa kutoona sinki na bomba la kunawia kabla ya kula, achilia mbali unakula nini maana nilikwisha jua tokea Bongo misosi kama ugali, supu ya makongoro, kisamvu, samaki mbasa wa ziwa Nyasa, dagaa wa Kigoma walopikwa kwa mawese na nyanya chungu nisingeweza kuipata abadani. Bila shaka na kile kipoza koo changu Castle Lager. Hakika huwezi kujua thamani ya kitu mpaka pale utakapokikosa.
“Kumbe watu hawa wachafu!” Nilitamka kimoyomoyo. Kabla ya kwenda semina Washington, DC pale Novemba nilitamani atokee malaika aninyakue na kunitua sehemu yoyote Bongo nikaendelee “kukamua’ na life lake. Nikapata matumaini mapya na kutiwa moyo pale nilipokutana na wa-Bongo wenzangu.
Fikiria ugumu wa miezi ya kwanza hapa Ughaibuni. Hakuna ndugu, marafiki, vyakula ulivyovizoea kama vile ugali na maharage ya Mbeya, daladala zilizojazana watu n.k. Falsafa yangu hata kabla na baada ya kuja hapa Mtoni ni kuwa hakuna sehemu duniani nitakapoweza kuitwa raia daraja la kwanza zaidi ya Bongo.
Sasa sina matatizo na kuzoea maisha hapa. Kila kitu “kama kawa” (mliokaa ughaibuni siku nyingi huu ni msimu uliozuka siku hizi kule Bongo kumaanisha “kama kawaida.” Hata misosi ya Kimtoni naitwanga, tuvinywaji nato si haba. Simba akizidiwa na njaa hata nyasi atakula tu.
Baada ya kuwafundisha wamarekani Kiswahili katika muhula huu wa kwanza rafiki yangu wa Alabama akaona si vema nikae mpweke katika kipindi hiki cha likizo ya mwisho wa mwaka. Akafanya “manuva” kunitoa New Jersey na kunileta Alabama, ambako nimefanikiwa kufungua blogu hii. Loh! Kama niko Bongo vile. Nimekutana na majamaa hapa lukuki yakiwa hayana hata mpango wa kurejea Bongo hivi karibuni. Ikiwezekana maisha yao yote kwani wengine wana wake na watoto hapa. Wengine wanaitisha kikao cha dharura kunifundisha namna ya kubakia Marekani. Michuzi anahitaji nguvu ya ziada kuwapemba hawa ndugu kurejea Bongo.
Breki ya kwanza ilikuwa kuuliza ugali uko wapi. Wakanipa kwa bamia, bilinganya na parachichi. Wanapokezana kunikirimu (sio kunipa takrima, ile rushwa ambayo Prez Jakaya anataka ifikiriwe na izungumzwe upya). Wananibeba kwenye magari yao makubwa kama lile la yule mbunge wangu kule Mbeya. Mimi sasa si tu mgeni wa Geofrey hapa bali wa wa-Bongo wote wa hapa Alabama. Nawashukuru sana kwa takrima yao hii wanayonionyesha.
Naongea nao na kuwasaili miaka waliyokaa hapa na wanaonaje maisha ya hapa ya kufanya kazi masaa 24 na kujirusha klabu za kucheza robo tatu uchi. Maisha kwao saaaaafi. Pia nawauliza kama wanajua kinachoendelea Bongo kisiasa. Si haba wanajua kuwa rais mpya ni Jakaya lakini ‘we don giv a shit who da hell da new PM iz.” Nawaambia ni Mzee Ngoyai. “Jamani vipi mpango wa kutafuta pesa na elimu hapa Marekani kisha kwenda kuwekeza na kufanya kazi Bongo ili tuiendeleze nchi yetu?” nawauliza.
“Men, whadashit iz dat? kurudi Afrika (hawasemi ‘Tanzania’ tena) kwenye mbu na inzi namna ile, rushwa, kodi isiyoonekana matumizi yake, daladala za kubanana katika joto la Dar es Salaam, barabara mbovu, na Ukimwi, hell no! Men, av come here to stay,” mmoja ananiambia kwa lahaja yake ya ki-kusini mwa Marekani na kuniacha njia panda kuhusu mimi kurejea Bongo.
Tuonane wakati mwingine.

7 Comments:

At 12:33 AM, Blogger mark msaki said...

mwaipopo!

ogonile

Men whada shit iz dat? umenifurahisha sana kwa kastori hako. umenifurahisa kwa kuwa mkweli pale ulipochangia mada ya kurudi nyumbani kwa bwana michuzi. kimsingi ni kuwa bwana kikwete na ngoyai wana kazi kubwa kuwahakikishia watanzania kuwa wao wako teyari kufanya kazi na watu wenye akili zao timamu na walio na majukumu ya kukabili maishani. kila mara huwa narudia hili suala la kuwaona watu binafsi - wanaojitegemea kama takataka, rushwa, mizengwe, kukosekana kwa demokrasia - uhuru wa kweli, na pia kuwanyima watu haki zao. nikikumbuka hili inaniuma sana hii habari ya madaktari wetu. unajua botswana ina madaktari wengi toka tanzania? je unajua ndio botswana inaonekana ni nchi inayofaa kuishi kuliko yetu, madaktari wetu wakichangia hilo? sio hilo tu kuna sekta nyingi ambazo Tanzania imeshindwa kuwashika watu na wataalamu wake kwa upendo na heshima.....tunamuomba michuzi na JKM warekebishe mambo watavyoona watu wanaingiza timu kwa spidi ya tsunami.....waache kusingizia kuwa watu wawe na wito kumbe wao wanawaona ni vibogoyo!!hakuna mtu aiyependa ndugu zake mkuu!!!

 
At 7:21 PM, Blogger Boniphace Makene said...

Mwaipopo huu ni mjadala niliokuwa nao muda si mrefu na Jeff. Nitaandika baadaye nilitaka kukusalimu tu. Pili mimi sikai Dar, natokea Musoma tena Vijijini huko ndiko alikoweka kakibanda kake Mzee Makene. Naona una harakati za kunikosanisha na wananchi. Kuna mengi Mwaipopo lakini je Tanzania ina utashi wa kutumia rasilimali za hawa ndugu zetu? Muulize Michuzi upya amekaa nje miaka mingapi na nini kilikuwa kisa? Nitaandika mazungumzo yangu na Jeff ambayo yaliambatana na kuungana na Ndesanjo kwa simu. Ya jana yalikuwa makali maana tulikuwa na Ernesto raia wa Kanada akionyesha uchungu na kuhoji nini kifanyike. Basi lala salama hapo Alabama, Baragumu linakuja kwa ukali na hii inanipa faraja.

 
At 1:27 PM, Blogger Jeff Msangi said...

Mwaipopo,
Kwa wengi hii inaweza kuonekana kama riwaya tamu tu ya kuvutia.Lakini pindi mtu anapotizama kwa undani atagundua kwamba kuna "ulemavu' wa akili miongoni mwetu.Mimi naanza na huo mbadiliko wa lafudhi.Najua masuala kama kutoga masikio,kuvalia suruali chini ya makalio,unywaji holela wa pombe,kujihusisha na madawa ya kulevya umeyaona huko ila kwa busara umemezea tu.Ni lazima vijana,tulio ndani na nje ya nchi yetu tujue fika kwamba hata siku moja Marekani,Canada,Uingereza na kwingineko ughaibuni hapawezi kuwa "nyumbani".A house is not a home(kiingereza kuweka msisitizo).Ndio maana hata ufanyeje wenye nchi yao huwa wanatuuliza "man,where are you from"?when are you going back home? nk.Hawatufukuzi ila wanatukumbusha kwamba pale si kwetu.Sasa tukitaka uhuru kamili,kuwa katika hilo daraja la kwanza lazima tufanye mambo haya.Tujiandalie mazingira ya kurejea makwetu,tupate elimu ya kutosha au mitaji ya kueleweka.Pili tupeleke changamoto kwa viongozi wetu watengeneze mazingira bora ya marejeo kupitia utawala bora,sera bora nk.Hizi nchi tunazogomea kwao(wengine bila hata vibali maalumu vya kuishimo) zimejengwa na watu.Kina nani?Na zetu je?

 
At 3:57 AM, Blogger Ndesanjo Macha said...

Hivi baada ule ugali uliokula una nini? Maana baada ya mlo ule umekuwa kimya. Najua ugali ukila unakupa nguvu mpya (na pengine ari mpya...sijui kama Kikwete ataendelea kula ugali)...ugali uliokula wewe ni tofauti nini?

Nakurushia dongo la chinichini!

 
At 10:13 AM, Blogger Boniphace Makene said...

Nakumbuka ugali alao mlevi mara nyingi humpa usingizi mzito. Kisha akiamka huja na fikra za kudhani kuna mtu kamuibia huku alikimbia mwenyewe kabla ya kulipa madeni! Una madeni nasi Mwaipopo maana hujatulipa ugali wetu kwa kurusha makala nyingine.

 
At 8:43 AM, Blogger Bwaya said...

Enyi mlio mbali, mwaweza kuleta mabaliko katika nchi yenu kuliko hata sisi wa hapa hapa. Nawatia moyo kuwa mnachokifanya si bure.
Navutiwa sana kuona kuwa umbali si hoja. Makene anasema mnawasiliana mara kwa mara na hata kutembeleana. Huo ndio uzalendo. Tuko wote na sisi tutafanya kinachotupasa, yaani kmuendeleza mijadala yenu miongoni mwa vijana.

 
At 1:23 AM, Blogger festo said...

wewe unasemaje utarudi huku au utakumbatia anasa na takrima za huko

 

Post a Comment

<< Home