Tuesday, January 24, 2006

Wanaume Mkae Chonjo, Wanawake Wamebumbuluka

Labda mwaweza kufikiri nimeivamia kazi ya Da’Mija kuhusu wanawake na maendeleo yao. Yawezekana ndivyo lakini mtazamo wangu umenituma nifanye hivyo. Ndesanjo naye jana kachokonoa.
Kadri dunia ibadilikavyo ndivyo hata mitazamo ya binadamu inabadilika. Hebu fikiri miaka ile ya zamani na sasa hasa katika ulingo wa siasa. Ilikua haba kukuta mwanamke eti yuko ngazi za juu kama vileza uraisi, umakamu wa raisi au hata uwaziri nyeti katika serikali, achilia mbali nchi za kifalme ambapo mtu anawezajikuta yu malkia ama mfalme midhali kazaliwa katika ukoo ama familia ya kifalme. Hata kama hana busara wala akili za kutosha anakua tu, utake usitake. Katika miongo na miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia mabadiliko ya mitazamo ya jinsia katika uwanja wasiasa duniani. Hata Afrika ambako mfumo dume umeshamiri (mfano kule mkoani Mara alikozaliwa Boniface Makene anayeishi Dar es Salaam). Tulikwisha zoea kuhusianisha majukumu ya kiserikali nawanaume. Katu hatukua hata na imani kuwa wanawake nao wanaweza. Sasa dunia imebadilika. Mtu wa jinsia yoyote iwayo anaweza kuwa kiongozi mkubwa tu katika siasa za ulimwengu huu pepe. Mwaka 1994 alianza Bibi Chandrika Kumaratunga wa SriLanka, Mwaka 2001 akafuatia Bibi Gloria Arroyo waPhillipines. Kama vile ndio waliwashamoto msululu wawanawake kutamani kuwa maraisi ukachanua. Hata katikaKenya aliwahi jitokeza Bibi Charity Ngilu lakini ghiliba za siasa za wakati ule katu hazikumwezesha kufua dafu mbele ya profesa Daniel arap Moi.
Wakinamamahawakuishia hapo. Mwaka jana kwa mara yakwanza mwanamama Angela Dorothy Markel, kiongozi yachama cha Christiaan Democratic Union alishinda kiti cha ukansela kule Ujerumani (pichani juu).
Mwaka huo huo mwanamama Ana Claudia Senkoro (pichani kushoto) kwa mara ya kwanza alikua mgombea wa kiti cha uraisi nchini Bongo. Hata hivyo, hakufanikiwa mbele yamidume ile 9 shababi yenye uchu wa Ikulu mithili yanini sijui. Mwaka huo huo 2005 katika mchuano mkali wa uraisi kule nchini Liberia kwa mara ya kwanza mwanamke mchumi Ellen Johnson-Sirleaf (chini ya Senkoro) alimbwaga mwanasoka George Opong Weah na kuwa raisi wa kwanza mwanamke katika Afrika nzima. Kama vile haitoshi kule Afrika ya kusini, baadaya aliyekuwa makamu wa rais Jakob Zuma kufanya maneno mbofumbofu, kwa mara yakwanza katika historia nzito ya nchi hiyo Mwanamama Phumzile Mlambo-Ngcuka aliteuliwa kuwa makamu wa rais wa nchi hiyo.

Mwezi huu kwa mara ya kwanza mwanamama Michelle Bachelet (kulia) amefanikiwa kuwa rais wa Chile mwanamke. Hapa Marekani kumekuwa na harakati za aliyekuwa mke wa raisi Clinton, Hillary Rodham Clinton kutamani kugombea na kuwa raisi wa kwanza mwanamke katikahistoria ya Marekani.

Ingawaje kule Bongo Prez Jakaya alishinda lakini nako mabadiliko ya jinsia si haba. Kwa mara ya kwanza katika baraza lake la mawaziri, ambalo kwa mara ya kwanza ni kubwa kuliko yote katika historia ya Bongo, amewateua wanawake wengi sio tu kuwa mawaziri bali pia kukamata wizara nyeti. Kwa mara ya kwanzaBibi Zakia Hamdani Meghji (kulia)amekuwa waziri wa kwanza wa pesa mwanamke katika Afrika ya Mashariki. Kwa mara yakwanza mhasibu Ana Makinda (kushoto) ameshinda na kuwa naibu wa Spika wa kwanza mwanamke. Kwa mara ya kwanza Mwanamke mwanasheria Dk Asha-Rose Mtengeti Migiro amekuwa mwanamake wa kwanza kuwa Waziri wa Mambo ya Kigeni na Ushirikiano waKimataifa.
Kwa mwendo huu dira inaonyesha wanamwake sasa wamebumbuluka baada ya kubumbulushwa. Na sasa hawasikii la mtu. Usawa kwa kwenda mbele. Enyi walume mnaofikiria kuingia katika siasa upinzani sasa ni waaina tatu: mosi dhidi ya wapinzani ndani ya chama, pili dhidi ya wapinzani nje ya chama, tatu dhidiyawanawake ndani na nje ya chama.

Thursday, January 19, 2006

Safari ya Alabama Ilifana Sana
Bila shaka wanablogu wa Kiswahili mmekuwa mkinikosa au kunimiss kwa wakati fulani hivi. Matatizo ya kiufundi yalinifungia nje ya ulimwengu wa blogu. Si shaka baadhi yenu mlikuwa mnafahamu nilikuwa Marekani ya kusini kule Hoover, Alabama kwa rafiki yangu Geofrey Mwaituka, ninayeonekana naye kwenye baadhi ya picha hizi. Huyo mwenje sweta jekundu ni mtoto wa Ilala Tonny Igata.

Hakika safari ya Alabama ilikuwa ‘bomba mbaya’ (nzuri). Tofauti na hapa New Jersey nilikorejea usiku wa jana, kule Alabama kuna wabongo kibao. Utafikiri watanzania huwa wanaambiana kuwa wao ‘waendage’ Alabama. Utafikiri hii haitoshi. Hali ya hewa kule ni bomba mbaya kama utaifananisha na hii ya hapa NJ. Kule kuna baridi ya afya sio hii ya dhoruba hapa karibu na New York.

Ingawaje wabongo wale hawatamani kurejea Bongo, hasa hivi karibuni, lakini kati ya majambo waliyonishauri nililipenda hili la kuwa wao hawawezi kurejea Bongo hivi sasa kwani hawajui namna ya kuanza maisha kule kwa Prez Jakaya na hivyo eti kwa kuwa mimi najua namna ya kuishi Bongo ni vema nimalizapo mizunguko ya hapa kwa Joji Kichaka nirejee Bongo. Wanadai ingawaje maisha yao ya hapa mtoni ni poa kinamna lakini wanayakosa maisha ya ndugu, jamaa na marafiki. Eti maisha ya hapa ni ya kikafiri tu. Basi tu kwa kuwa wamesha yazoea. Wafanyeje?

Nimechomekea kiduchu muhtasari wa mtazamo wa maisha ya hapa Marekani ingawaje sio lengo kuu la chapisho hili. Leo natamani kuwasabahi tu. Naona Boniface Makene na Ndesanjo Macha walishaanza-ga kuwa-ga na wasiwasi kuwa huenda nilishapotelea Mexico. Nimerejea na ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya ya ugali wa kule kusini mwa nchi hii. Kublogu kwa kwenda mbele.

Sunday, January 01, 2006

Nimekula Ugali Alabama

Tangu nilipopata ufahamu wa kutambua jema na baya, nimekuwa na njozi ama ndoto za aina aina. Nikiwa mdogo bila shaka nilianza kufikiri kuwa mtu fulani hapo nitakapokuwa mtu mzima (ukiwa mdogo unakuwa kipande?). Kama mtu mwingine yeyote wakati huu mtu hufikiria mathalani kuwa daktari, mwalimu, dereva, askari polisi na kadhalika. Pia wakati mwingine hufikiria kupata vipawa na uwezo wa kufanya mambo kadhaa pale wasaa utakapowadia mfano kuoa ama kuolewa, kupata watoto ama hata kusafiri kwenda mikoa hata nchi za mbali.
Baada ya njozi zangu za utotoni na ujanani kutokea kweli na zingine kubakia kuwa za alinacha tu, hatimaye ile ya kisafiri nchi za mbali ilitimia mwaka tulioumaliza hivi punde pale mwezi wa tano nilipoletewa mkataba Mbeya ili niusaini kukubali ama kukataa kuja hapa kwa Mzee Joji kudurusu Kiswahili. Kama ilivyo kwa wa-Bongo wengi wasaa wa kuja Marekani hufuatia ule wa kwenda mbinguni kwa umaarufu. Nani akatae kuja Mtoni? Nikiwa na mchanganyiko wa bashasha na huzuni ya kuiacha kazi ya kufundisha kule nyumbani Mbeya, hatimaye nilikanyaga udongo wa wababe wa dunia pale mwezi wa nane. Nikiwa na shauku ya kukuta mambo mema mengi hapa Marekani, kwangu ulikuwa wakati mgumu kuiacha kazi niliyokuwa nimeizoea na marafiki zangu wa haja. Sikukumbuka hata kumuaga bibi yangu Ndimbumi Kafwila kule Kyela. Mungu awalinde hata tutakapokutana tena.
“La haula lakwata! Kumbe Marekani iko hivi!” Ndiyo yaliyokuwa maneno nilijisikia kuyasema pale ile ndege iliyoninyakua Afrika ya Mzee Mandela ilipokuwa ikielekea kutua jijini Atlanta. Kama watu wengi wadhaniavyo, hakika mandhari ya nchi hii yalisema karibu ndugu Mwaipopo hapa Mtoni ufurahie kutokuwepo kwa mbu na inzi, ufurahie barabara za orofa, umeme na maji visivyokatika kama Dar es Salaam anakokaa Boniface Makene na Muhidin Issa Michuzi. Hakuna haja ya kuyaorodhesha sana maajabu ya hapa Marekani.
Nikawa katika “nchi ya ahadi" katika jimbo la New Jersey. Siku ya kwanza mgahawani nikashangaa kutoona sinki na bomba la kunawia kabla ya kula, achilia mbali unakula nini maana nilikwisha jua tokea Bongo misosi kama ugali, supu ya makongoro, kisamvu, samaki mbasa wa ziwa Nyasa, dagaa wa Kigoma walopikwa kwa mawese na nyanya chungu nisingeweza kuipata abadani. Bila shaka na kile kipoza koo changu Castle Lager. Hakika huwezi kujua thamani ya kitu mpaka pale utakapokikosa.
“Kumbe watu hawa wachafu!” Nilitamka kimoyomoyo. Kabla ya kwenda semina Washington, DC pale Novemba nilitamani atokee malaika aninyakue na kunitua sehemu yoyote Bongo nikaendelee “kukamua’ na life lake. Nikapata matumaini mapya na kutiwa moyo pale nilipokutana na wa-Bongo wenzangu.
Fikiria ugumu wa miezi ya kwanza hapa Ughaibuni. Hakuna ndugu, marafiki, vyakula ulivyovizoea kama vile ugali na maharage ya Mbeya, daladala zilizojazana watu n.k. Falsafa yangu hata kabla na baada ya kuja hapa Mtoni ni kuwa hakuna sehemu duniani nitakapoweza kuitwa raia daraja la kwanza zaidi ya Bongo.
Sasa sina matatizo na kuzoea maisha hapa. Kila kitu “kama kawa” (mliokaa ughaibuni siku nyingi huu ni msimu uliozuka siku hizi kule Bongo kumaanisha “kama kawaida.” Hata misosi ya Kimtoni naitwanga, tuvinywaji nato si haba. Simba akizidiwa na njaa hata nyasi atakula tu.
Baada ya kuwafundisha wamarekani Kiswahili katika muhula huu wa kwanza rafiki yangu wa Alabama akaona si vema nikae mpweke katika kipindi hiki cha likizo ya mwisho wa mwaka. Akafanya “manuva” kunitoa New Jersey na kunileta Alabama, ambako nimefanikiwa kufungua blogu hii. Loh! Kama niko Bongo vile. Nimekutana na majamaa hapa lukuki yakiwa hayana hata mpango wa kurejea Bongo hivi karibuni. Ikiwezekana maisha yao yote kwani wengine wana wake na watoto hapa. Wengine wanaitisha kikao cha dharura kunifundisha namna ya kubakia Marekani. Michuzi anahitaji nguvu ya ziada kuwapemba hawa ndugu kurejea Bongo.
Breki ya kwanza ilikuwa kuuliza ugali uko wapi. Wakanipa kwa bamia, bilinganya na parachichi. Wanapokezana kunikirimu (sio kunipa takrima, ile rushwa ambayo Prez Jakaya anataka ifikiriwe na izungumzwe upya). Wananibeba kwenye magari yao makubwa kama lile la yule mbunge wangu kule Mbeya. Mimi sasa si tu mgeni wa Geofrey hapa bali wa wa-Bongo wote wa hapa Alabama. Nawashukuru sana kwa takrima yao hii wanayonionyesha.
Naongea nao na kuwasaili miaka waliyokaa hapa na wanaonaje maisha ya hapa ya kufanya kazi masaa 24 na kujirusha klabu za kucheza robo tatu uchi. Maisha kwao saaaaafi. Pia nawauliza kama wanajua kinachoendelea Bongo kisiasa. Si haba wanajua kuwa rais mpya ni Jakaya lakini ‘we don giv a shit who da hell da new PM iz.” Nawaambia ni Mzee Ngoyai. “Jamani vipi mpango wa kutafuta pesa na elimu hapa Marekani kisha kwenda kuwekeza na kufanya kazi Bongo ili tuiendeleze nchi yetu?” nawauliza.
“Men, whadashit iz dat? kurudi Afrika (hawasemi ‘Tanzania’ tena) kwenye mbu na inzi namna ile, rushwa, kodi isiyoonekana matumizi yake, daladala za kubanana katika joto la Dar es Salaam, barabara mbovu, na Ukimwi, hell no! Men, av come here to stay,” mmoja ananiambia kwa lahaja yake ya ki-kusini mwa Marekani na kuniacha njia panda kuhusu mimi kurejea Bongo.
Tuonane wakati mwingine.

Wednesday, December 28, 2005

Asalam aleikum

Asalaam aleikum waungwana wote waandishi na wasomaji wa blogu za Kiswahili na nyinginezo. Ama hakika mvuvumko wangu leo waanzia hapa kwenye jukwaa hili la kupashana na kujadili habari na masuala anuai. Bila ya kuchelewa, nimekuwa nikicheza ngoma hii kwa kutazama na kukodolea macho nikiwa nimejikunyata pembezoni mwa kiwanja (wengine husema uwanja). Yawezekana kabisa baadhi yenu mmepiga chabo nomino langu likitokea katika kuchangia hili ama lile.

Awali ya yote mie ni miongoni mwa wale tunaosapoti 'blog' ziitwe 'blogu', 'blogger/bloggers' tuite 'wana/mwanablogu.' Au mwasemaje. Niliwahi kuchangia hili la neno la blog kwa Kiswahili katika blogu ya Jeff. Baada ya kuwa nimefanya hivyo nikabahatika kuendelea kufanya utafiti wa maneno mengine ambayo tumebomu kutoka viluga vingine. Nimefanikiwa kupta maneno ya wingi wa haja tu lakini leo nitawapa moja ambalo limenishangaza kwa kweli. Jamani lugha haibadiliki kama tarehe. Kumbe hata neno 'bamia, ile mboga inayoteleza mdomoni, tulilitoa uarabuni!

Boniface Makene amekuwa haishi kunipemba eti nami nijiunge kilingeni. Kuandika na kuandika-andika havitangamani. Ndesanjo naye hakua kando katika kushadidia hamasa hii niliyokua nayo dahari za siku nyuma ingawaje msongo wa shule na kazi na mambo kadha wa kadha vilifanikiwa kunivuta nyuma. Hayawi hayawi, basi yaelekea sasa yanaweza kuwa yanakua.

Kutamani kuwa na ka-blogu kangu na kuweza kukafanya kadumu ni vitu viwili tofauti. Kumbe kwa kuwa maji nimeshayavulia salawili basi sina haja ya kuyachumpia ili kuyaogelea. Si haba nanyi sasa mwaweza kuwa mkipata pahala pa kutembelea japo mara moja kwa muda fulani.

Twende Kazi